Pages

WORD


SOMA NENO, TAFAKARI NENO, TENDA NENO
By CLEMENT EMMANUEL a.k.a RICH IN JESUS
Mobile no: 0717740706 & 0752570017
blog : yotekwayesu.blogspot.com
SALAMU ZA AWALI KABLA YA SOMO
BWANA Yesu apewe sifa sana ndugu mpendwa! mimi binafsi najisikia furaha sana kiasi kwamba nashindwa hata kuelezea. Nina furaha kubwa kwa sababu bwana Yesu ameamua yeye mwenyewe kukufikia wewe ndugu msomaji kupitia somo hili, ambalo alianza kunifundisha mimi kwanza kwa uwezo wa Roho wake Mtakatifu, kisha akanipa kibali niweze kukufikia pia wewe ndugu yangu msomaji, ili sote tupate kuzingatia maagizo yake kisha tuweze kupata mafanikio hapa dunia kisha kuingia katika uzima wa milele.
Mimi binafsi ninamrudishia sifa Mungu kupitia mwanawe mpendwa Yesu kristo BWANA na mwokozi wa maisha yangu. Kwani ndiye aliyekiandika kitabu hiki yeye mwenyewe kupitia uwezo wa Roho Mtakatifu wake akaaye ndani yangu. Roho Mtakatifu msaidizi wangu mwema, Amekuwa mwaminifu mno akinielekeza mimi kama chombo tu ni kitu gani niandike ili makusudi ya Mungu yatimizwe juu yako wewe ndugu msomaji.
Ninajua ya kwamba shetani hapendi kabisa wewe unayesoma kitabu hiki upate ufahamu juu ya maneno ya Mungu, tena hapendi kabisa upate kuelewa mawazo mema ya Mungu juu ya maisha yako. Kwani anajua mafanikio ya maisha yako yanatoka kwa Mungu pekee, pia siri zote za maisha zipo kwenye NENO la Mungu pekee. Sasa ninajua shetani ambaye ni baba wa uongo na jeshi lake wamejipanga vizuri sana kukuzuia usiweze kujua siri za ufalme wa mbinguni kupitia kitabu hiki. Lakini kwa jina la Yesu kristo lipitalo majina yote (wafilipi 2:9-11), ninakuamuru shetani umwache ndugu msomaji anayetaka kusoma siri hizi na ukimbilie kuzimu ukateketee huko kwa mamlaka ya jina laYesu kristo, kwani imeandikwa katika (ufunuo 12:11) ya kwamba “Nao wakamshinda kwa damu ya mwana-kondoo,.…..”, nami sasa kwa damu ya Yesu kristo ninazitakasa fahamu za ndugu msomaji na ninakuamuru wewe shetani katika jina lipitalo kila jina, jina la Yesu kristo! uziache kabisa fahamu za ndugu msomaji, ili msomaji apate kuelewa siri ambazo Mungu ameziweka leo mbele yake kupitia kitabu hiki.
Ndugu msomaji katika jina la Yesu! Ninakukaribisha sasa ili tuweze kutafakari kwa pamoja maneno ya Mungu, ila nakusihi usome kwa kutafakari na ninakuhakikishia ya kwamba msaidizi wetu Roho Mtakatifu yupo nawe hivi sasa, ili kukusaidia wewe ndugu msomaji uweze kuelewa na kuyatendea kazi maneno ya Mungu utakayosoma katika kitabu hiki.
HEBU SASA NA TUANZE SOMO LETU KWA PAMOJA, KATIKA JINA LA YESU!  




NDUGU YANGU MPENDWA KATIKA JINA LA YESU KRISTO WA NAZARETI ALIYE HAI,  NAOMBA TUANZE SOMO LETU KWA KUJIULIZA MASWALI YAFUATAYO ;-
Ø  NENO NI NINI?
Ø  KWA NINI TUSOME NENO?
Ø  JE NI KWELI TUKISOMA NENO, TUNAMSOMA YESU?
Ø  NINI HASARA YA KUTOSOMA, KUTOTAFAKARI NA KUTOTENDA NENO?
Ø  NINI FAIDA YA KUSOMA, KUTAFAKARI NA KUTENDA NENO?
Ø  KIPI BORA! FAIDA AU HASARA?




NENO NI NINI ?
Neno ni mkusanyiko wa herufi ambazo zikiunganishwa zinetengeneza maandishi ambayo yanaleta maana kwa msikilizaji au msomaji wa maandishi hayo, au tafsiri nyingine ya neno inasema, Neno ni mazungumzo yanayolenga kuelezea kitu Fulani, au wengine hutafsiri kwa kusema, Neno ni maagizo yatolewayo kwa mtu kwa njia ya maandishi au kwa njia ya mazungumzo. Najua unaweza ukawa na tafsiri nyingi mno za neno kwa kadiri unavyoelewa, mimi ninajua ya kwamba upo sahihi kabisa kwa tafsiri ulizo nazo. Lakini mimi nimeona ni vema tuzitumie hizi chache nilizoziandika katika kitabu hiki.
Mimi ningependa tuangalie tafsiri ya neno kama, “maagizo yatolewayo kwa mtu kwa njia ya maandishi au kwa njia ya mazungumzo, yakilingenga kuelezea kitu Fulani chenye manufaa kwa msomaji au msikilizaji, Ili tu aweze kupata kuelewa na mara nyingine uweze kutenda kitu kilichokusudiwa ndani ya mazungumzo hayo” kwa mfano mtu akikwambia neno imba! Mtu huyo anatarajia kukuona ukiimba, usipoimba inamaanisha ya kwamba; pengine hujasikia neno hilo au umeacha kutenda sawa sawa na neno hilo.
NENO LA MUNGU unaweza ukaritafsiri kama maana nyingine za neno lakini tofauti kubwa iliyopo ni kwamba neno la Mungu li hai na mtu akilizingatia na kulitenda linamletea usitawi na mafanikio kama linavyosema neno la Mungu katika Joshua 1:8.
Sasa basi ni vema wewe ukatambua kwamba Mungu wetu huwa hafanyi kitu ambacho kipo nje ya neno lake, ndio maana katika yeremia 1:12b Bwana akasema “kwa maana NINALIANGALIA NENO LANGU, ILI NILITIMIZE ”
Kwa hiyo neno la Mungu ni la  muhimu sana kwa maisha bora ya mkristo yeyote asiyetaka kuangamia kwa kukosa maarifa, kwani hosea 4:6 inasema ya kwamba “watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa;……………………………………….”



KWA NINI TUSOME NENO?
Katika hali ya kawaida ukuaji wa kiumbe chochote hutegemea sana ni vitu gani anavyokula, sasa basi ili kiumbe hai yeyote akue vizuri anatakiwa ale chakula kilichokamilika yaani kwa kiingereza (balanced diet) ili apate kuwa na afya njema.
Ukitaka kuangalia ukuaji wa kiumbe hai chochote  hasa binadamu angalia ni vyakula gani anavyokula. Akiwa na afya mbaya, sisi tutajua tu kwamba chakula anachokula kina mapungufu au labda pengine huwa anakula kwa shida sana na ndio maana anadhoofika.
Akiwa na afya nzuri tutajua tu ya kwamba binadamu huyu anakula chakula bora na chenye virutubisho vyote muhimu kwa afya yake.
Sasa basi kama ukuaji wa binadamu kimwili hutegemea chakula bora. Basi pia ukuaji wa binadamu kiroho hutegemea chakula bora chenye virutubisho vyote kiroho yaani NENO la MUNGU litokalo kwenye kinywa cha MUNGU ambalo siku zote hutimiza mapenzi ya mungu (Isaya 55:11).
Labda nikumegee siri kidogo ndugu yangu ya kwamba “ AMINI USIAMINI MAFANIKIO YAKO YOTE YAPO KWENYE NENO LA MUNGU yaani MAANDIKO MATAKATIFU”.
Mtu mwingine anaweza asielewe kabisa kwamba mafanikio yake yote yapo kwenye neno la MUNGU, aah! ndugu yangu mpendwa. Mimi binafsi nilianza kuona mafanikio mengi kwenye maisha yangu ya wokovu, baada ya kuanza kulisoma na kulitafakari neno la MUNGU lakini kabla ya hapo nilikuwa ninajiona nipo kawaida sana yaani nilikua na utapia mlo wa kiroho ambao ulizuia mafanikio yangu katika Nyanja zote za kimaisha yaani kiroho na kimwili. Hehu jiulize ni kwa nini MUNGU alimwambia Joshua mwana wa Nuni ya kwamba “kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali YATAFAKARI maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia KUTENDA sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; ndipo UTAKAPOIFANIKISHA njia yako, kisha ndipo UTAKAPOSITAWI sana” Joshua 1:8 . sasa hebu tujiulize kwa pamoja ni kwa nini MUNGU katika maagizo yake ya kwanza kabisa kwa Joshua aamue kumsisitizia habari ya umuhimu wa  maneno ya torati juu ya kufanikiwa na kusitawi katika kila  alilolifanya, Ni kwa nini asingembwambia fanya maombi sana au sifu sana?. Naomba uelewe vema kabisa ya kwamba NENO LA MUNGU linabeba kila kitu cha KIMUNGU ambacho kinapelekea mafanikio yote ya KIMUNGU pia. Kwa sababu kama ni maombi yameandikwa kwenye neno kama ni sifa na kuabudu vipo kwenye neno kama ni ndoa inafundishwa kupitia neno, kama ni hekima inapatikana kupitia neno la Mungu, kwa kifupi neno ni kila kitu kwa mtu anayetarajia kwenda mbinguni yaani MLOKOLE.
Ni wazi kabisa ya kwamba Joshua asingezingatia torati inasema nini juu ya safari ya wana wa Israeli pengine kaanani(nchi ya ahadi) ingekuwa ndoto kwa wana wa Israeli. Ndio sijakosea! namaanisha kaanani ingekuwa ndoto kwa wana israeli, pengine na kwako pia ukiliacha neno la Mungu MBINGUNI utapasikia kwenye redio tu. 
Si hivyo tu ukiacha kusoma neno la MUNGU, pia ukiacha kutafakari neno na tena ukiacha kutenda sawa sawa na neno la MUNGU, mafanikio kwako itakuwa shida na kusitawi kwako kunaweza kukawa na matatizo mengi na mashaka ndani yake. Ndio maana leo roho mtakatifu ameamua kukukumbusha ya kwamba SOMA NENO,TAFAKARI NENO, TENDA NENO!
Hebu tuangalie pia Zaburi 119:105 “neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia zangu ” ukiangalia maneno hayo ya zaburi utagundua ya kwamba usipolijua neno la MUNGU miguu yako na njia zako zitakuwa giza totoro. Sasa basi ukitaka mwaga pia taa ikuwakie katika maisha yako yote ni vema ukachukua taa hii yaani neno kwani taa hii haiishiwi nguvu hata siku moja.
Ukiangalia pia mithali 16:20a “Atakayelitafakari neno atapata mema;” sasa basi naomba ujue ya kwamba hakuna mema yoyote pasipo neno, mtu mwingine anaweza akajiuliza maswali  mengi akakosa majibu, ila ndugu yangu ngoja tu nikueleze ya kwamba, kila unachokitafakari sana ndicho mara nyingi unachokipata sasa na baadae. Sasa basi ni bora sana tena sana wewe uamue leo kutafakari neno la Mungu lenye pumzi ya uhai ili  upate mema yote yaliyozungumzwa humo (yaani kwenye biblia),




JE NI KWELI TUKISOMA NENO, TUNAMSOMA YESU?
Ndio hii ni kweli kabisa! Tukisoma neno twamsoma YESU!, yaani tukisoma neno tunamsikia YESU anavyotuagiza juu ya maisha yetu, kwa sababu YESU ni NENO. Ha! Hii ni kweli jamani!? Ninajua ni jinsi gani unavyojiuliza maswali mengi ambayo yanakusumbua kupata majibu yake mara moja, ila mimi nikwambie ya kwamba kwa kuwa ROHO MTAKATIFU ni msaidizi wako naye yupo nawe hapo wakati unatafakari kitabu hiki, ninajua atakusaidia kuyaelewa haya.
Sasa basi hebu twende kwa kuyaangalia kiundani maneno ya Mungu, Roho mtakatifu akitusaidia. JE NDUGU YANGU UPO TAYARI TUANZE? Haya hebu fungua kitabu cha yohana 1:1-5. Utakuta maneno haya “hapo mwanzo kulikuwepo Neno, naye Neno alikuwa kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. ……………………………………………”, haya hebu turuke na tusome yohana 1:14, ambapo utakuta maneno haya “naye Neno alifanyika mwili. Akakaa kwetu: nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli”. Hivi ndugu yangu, je ni nani aliyefanyika mwili akakaa kwetu?, ni nani mwana pekee wa Baba?, je YESU siye NENO ambaye alikuwa MUNGU?. YESU ndiye NENO kutokana na maandiko ya yohana tuliyoyasoma. Ndugu mpendwa mimi ninajua ya kwamba Roho mtakatifu kwa wema wake amekufundisha vizuri kabisa Nawe umeelewa vema.
 Lakini ndugu yangu hebu pata shauku ya kuendelea kuyachunguza maandiko na kuyatafakari zaidi ili Roho mtakatifu msaidizi wetu mwema azidi kusema nawe kiundani zaidi kwa sababu MUNGU huwapenda watu wachunguzao maandiko kila siku, soma matendo 17:11 “watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa thethalonike, kwa kuwa walipokea lile neno kwa ulekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo.”  Sasa basi hebu nawe zingatia kuyachunguza maandiko KILA SIKU ili upate kuelewa kiundani MUNGU anasema nini nawe.
Angalia tena ufunuo 19:13-16 ”naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, NENO LA MUNGU ……………………………………………………………………………… naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA BWANA WA MABWANA.”  Je ni nani aitwaye MFALME WA WAFALME?, tena ni nani aitwaye BWANA WA MABWANA?. Ninajua utakuwa haujapishana sana na ukweli, na pia jibu lako litakuwa ni “YESU”. Sasa basi hebu rejea mstari wa 13b NA JINA LAKE AITWA, NENO LA MUNGU. Sasa nadhani umeelewa ya kwamba ukisoma NENO unamsoma YESU moja kwa moja.
Ndugu yangu kutokana na jinsi tulivyoona hapo juu na jinsi Roho mtakatifu anavyozidi kukukumbusha naomba uamini sasa kwa jina la YESU kristo wa nazareti aliye hai jina lipitalo majina yote, ya kwamba “Unavyopata muda wa kutafakari Maneno ya Mungu (Biblia), unapata muda wa kumsikiliza YESU mwenyewe anasema nini kwenye maisha yako. Na ukitenda sawa sawa na maneno ya Biblia takatifu (neno la Mungu), utakuwa unatenda sawa sawa na YESU anavyotaka wewe utende.
Ndugu yangu kumbuka kusoma neno! Kutafakari neno! Na kutenda neno, Kwa maana nyingine utakuwa unamsoma yesu anavyokuagiza ndani yako! Kisha unamtafakari yesu! Halafu unatenda Kama yesu anavotaka utende, ELEWA YA KWAMBA ukizingatia neno la Mungu utapata kufanikiwa na kusitawi sana, kwa sababu hakuna jambo lolote chini ya jua ambalo halipo kwenye neno la Mungu, Kila kitu kipo kwenye neno la Mungu.
Shetani anafanya kila jitihada kuhakikisha kwamba wewe husomi neno na ukisoma huelewi na ukielewa hutendi kama neno linavyokuagiza, kwa sababu anajua MAFANIKIO YAKO YAPO KWENYE NENO LA MUNGU. 
Ndugu yangu SOMA NENO, TAFAKARI NENO, TENDA NENO! Nawe utapokea vingi kutoka kwa BWANA, elewa kwamba NENO ndilo pekee litasimama mambo yote yatapita lakini neno tu ndilo litadumu, Kwa maana nyingine YESU pekee atasimama. Soma 1Petro 1:23-25





NINI HASARA YA KUTOSOMA, KUTOTAFAKARI NA KUTOTENDA NENO ?
  1. UTAANGAMIA KIROHO NA KIMWILI
Ukisoma Hosea 4:6 utakutana na maneno “watu wanguwanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako”, sasa hapa ndugu yangu unaweza kugundua kitu kimoja ya kwamba Mambo ambayo walizuiliwa yalitokana na wao kukosa maarifa na ambayo yalizungumzwa kwamba yatokana na Neno la Mungu  kama mistari ya mwanzo kabisa ya hosea katika sura ya nne inavosema “lisikieni NENO la BWANA,………………………..” unaweza ukagundua ya kuwa kuangamia kwa watu wake Mungu kunatokana na kutokulisikia neno la BWANA, kwani ukiendelea kuangalia mistari ya mwanzoni kabisa inayoendelea hapo chini katika sura ya nne utaona kuwa kwa kutokulisikia neno la BWANA nchi iliingia katika dhambi kama “kuapa kwa uongo, na kuvunja ahadi, na kuua, na kuiba, na kuzini…………”, sasa ukijaribu kuanzalia kitabu hiki cha Hosea utaona ya kwamba nchi ile ilitenda dhambi sana, hasa hasa dhambi ya uzinzi na iliacha kusikia neno la bwana, ndio maana BWANA akawasikitikia kwa kuangamia kwao kwa sababu yeye hapendi watu wake waangamie ndio maana akaamua kumtuma Yesu kristo mwana wake wa pekee ili kila amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele (yohana 3:16), sasa basi hebu jaribu tena kuangalia katika mstari wa sita wa hosea kwa makini kisha uutafakari kiundani ukimwomba Roho Mtakatifu akusaidie, ukiutafakari vizuri utagundua ya kwamba ukikataa maarifa ya Mungu, MUNGU ATAKUKATAA PIA, KISHA ATAWASAHAU WATOTO WAKO; sasa angalia hasara ya kutotafuta maarifa ya BWANA kupitia NENO LAKE TAKATIFU(BIBLIA), yaani kukataliwa kutaanza kwako wewe kwanza kisha kutaendelea mpaka kwa watoto wako! Ndio sijakosea namaanisha ya kwamba, kutaendelea mpaka kwa watoto wako.
Hebu jiulize swali lifuatalo ndugu yangu, “Hivi haya mambo yaliyowasababisha watu wa Mungu waangamizwe je hayapo kwenye amri kumi za Mungu?”, jibu ni rahisi tu ndugu yangu, mambo hayo yote yameandikwa kwenye amri kumi. Hebu soma mwenyewe kitabu cha Kutoka 20:1-17 na kumbukumbu 5:6-21. Hebu tujiulize tena sasa “hivi kama amri zipo na watu wanaangamizwa na kama neno lipo na watu wanaangamizwa, maana yake ni nini?”. Maana yake ni kwamba watu wenyewe wanataka kuangamizwa  kutokana na ukweli kwamba neno la Mungu limewekwa wazi kwa kila mtu anayetaka kulijua na kila mtu anayetaka kufanikiwa na kusitawi (yoshua 1:8).
Shetani baba wa uongo anajitahidi sana kukudanganya ili usipate muda wa kusoma neno na kutafakari neno, kwa sababu anajua silaha mojawapo ya mafanikio yako kimwili na kiroho ni NENO LA MUNGU, soma waefeso 6:17b “na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu”. Hivi wewe unafikiri shetani ni mjinga sana eeh! Eti akuachie tu wewe uwe na UPANGA WA ROHO ili umkate na kumuua kabisa, hapana ni lazima apigane nawe kwa kiasi kikubwa na ahakikishe ya kwamba hupati muda hata kidogo wa kuangalia neno la Mungu. Naomba utambue ya kwamba mafanikio yako ya kimwili yanaanza na mafanikio yako ya kiroho, soma mwenyewe 3Yohana 1:2 utakuta maneno haya “mpenzi naomba UFANIKIWE katika mambo YOTE na kuwa na afya yako, kama vile roho yako IFANIKIWAVYO”, sasa ukubali ukatae hii ni kanuni ya kiMungu ya kwamba, unataka ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako (kimwili) ni lazima uanze kutakuta kuwa na mafanikio kiroho kwanza, kwa hiyo kama unataka shetani asikushinde katika mambo yote ni lazima utafute kwanza UPANGA WA ROHO yaani NENO la Mungu, tena sio utafute tu likae kinywani mwako, ulitafakari naulitende (yoshua 1:8), ooooh HALELUYA mtu wa Mungu!, Nakusihi usiache kuyatendea kazi haya maneno ambayo Roho anakuambia hivi sasa.


  1. HUTAPATA MAJIBU YA MAOMBI YAKO
Mtu mwingine anaweza asikubalie kabisa na jambo hili na wala asielewe kabisa kwamba majibu ya maombi yote ayaombayo hutokana na jinsi gani mtu amelijaza neno la Mungu ndani yake, najua suala hili limekuwa likikusumbua kwa kiasi kikubwa kwani hata mimi lilinisumbua sana, lakini ninamshukuru Yesu wangu kwa wema na fadhili zake kwani aliamua kunifundisha yeye mwenyewe kupitia uwezo wa Roho Mtakatifu ambaye ndiye msaidizi wetu, ndio maana leo ameamua kukufundisha na wewe ili ukiomba upokee majibu yako pasipo na shaka yoyote, ila kabla hatujaangalia maandiko nasikia roho mtakatifu akinikumbusha nikwambie ya kwamba majibu ya maombi yako hayatatokana tu na kulijaza neno pekee bali kulitenda na kuzingatia maagizo akupayo msaidizi wako Roho Mtakatifu.
Sasa hebu tuangalie kitabu cha Yohana 15:7 ambapo tutakutana na maneno yafuatayo”ninyi mkikaa ndani yangu, na MANENO YANGU yakikaa ndani yenu, OMBENI mtakalo lote nanyi MTATENDEWA”, ndugu yangu katika jina la Yesu kristo wa nazareti aliye hai ninamwomba Roho Mtakatifu akusaidie upate kuelewa vizuri na akuwezeshe ili macho yako ya rohoni yapate kutiwa nuru kabisa na ujue kusudi la Mungu kuweka kitabu hiki mbele yako.
Sasa hebu tutafakari kwa pamoja maneno haya ya Mungu yaliyoandikwa katika kitabu cha Yohana mtakatifu, utaona Yesu anasema ya kwamba “ninyi mkikaa ndani yangu”, yaani wewe ndugu yangu msomaji ukikaa ndani ya Yesu kabisa kabisa na ukijitoa kuwa mali ya Yesu yaani UKIOKOKA, na situ kuokoka pekee bali ukitenda kama Yesu anavyokuagiza utende, basi utajibiwa maombi yako pasipo shaka yoyote.
Kwa sababu ni lazima uelewe ya kwamba huwezi kukaa ndani ya YESU halafu eti bado Ukawa MZINZI, MLEVI, MCHAWI, FISADI na namna nyingine mbaya ambazo unazo na Roho Mtakatifu anakushuhudia ya kwamba ni mbaya. Hebu soma mwenyewe Wagalatia 5:19-21 utayaona matendo ambayo ukiwa nayo huwezi kukaa ndani ya Yesu.
Lakini ukiwa na matendo mema kama UPENDO,FURAHA,AMANI na mengine mengi mazuri kama yalivyoandikwa katika kitabu cha Wagalatia 5:22-23 utakaa ndani ya yesu na kupata manufaa mengi ambayo yapo kwa Yesu kristo wa nazareti aliye hai, Acha tu nikwambie ndugu yangu ya kwamba ukiwa ndani ya Yesu unapata uwezo wa kufanyika mwana wa Mungu (yohana1:12),  pia unakuwa rafiki wa Yesu (yohana 15:14-15) na zaidi sana Roho mtakatifu anapata kibali cha kukaa ndani yako na kukusaidia katika mambo yote (1wakorintho 3:16).Sasa wewe unasubiri nini kumpokea Yesu? Mimi nakushauri amua sasa kumpokea Yesu ukimaanisha kabisa kutoka ndani ya Roho yako, na kufuata sala ambayo itakuwa mwishoni kabisa mwa kitabu hiki kwa uwezo wa Roho mtakatifu.
Ila sasa kumbuka ya kwamba Yesu hakuishia tu kusema maneno“ninyi mkikaa ndani yangu” pekee, bali aliendelea tena kwa kusema “na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa”, sasa ni lazima uelewe ya kwamba, kutendewa kwako katika hayo maombi unayoomba kunatokana kabisa na kuyaweka maneno ya Mungu kwa wingi ndani yako, ndio maana akasisitiza “na maneno yangu yakikaa ndani yenu” halafu akamalizia “ombeni mtakalo lote mtatendewa”.
Sasa mimi binafsi nakushangaa wewe usiyetaka kusoma, kutafakari na kutenda neno la Mungu halafu unatarajia majibu ya maombi yako, ndio eeh! Mimi nakushangaa kabisa kabisa, halafu baada ya kukushangaa naona ni vema nikushauri ili watu wengine wasikushangae sana, na ushauri wangu kwako ni kwamba “SOMA NENO, TAFAKARI NENO, TENDA NENO”, halafu uone kama hujajibiwa maombi yako!, mimi nakuhakikishia kwa jina la Yesu kristo wa nazareti aliye hai ya kwamba ni lazima ujibiwe hayo maombi yako, kwa sababu mimi binafsi nilijibiwa na na naendelea kujibiwa mengi niliyoyaomba baada ya kugundua kanuni hiyo.



  1. UTALAANIWA
“Na alaaniwe asiyeyaweka imara maneno ya torati hii kwa kuyafanya. Na watu wote waseme, amina ”,Kumbukumbu 27:26, ukijaribu kuyachunguza vizuri maneno haya ambayo yameandikwa kwenye kitabu cha tano Musa cha kumbukumbu la torati. Utagundua ya kwamba, Mungu alipenda kuwapa maagizo wanaisraeli moja kwa moja kupitia mtumishi wake musa, ili kwa yeyote atakayetaka kuyafuata maagizo ya Mungu basi awe salama, na kwa atakayekaidi apate ujira wake wa laana pia.
Sasa hebu sikia maneno haya na uyatafakari kwa makini, “na alaaniwe!”  Mmh! ndugu yangu, hebu tujiulize ni nani alaaniwe?. “Asiyeyaweka imara maneno ya torati!”. Eeeh! Kumbe usipoyaweka imara maneno ya torati ni wazi kwamba unataka laana, sasa utayawekaje imara maneno ya torati? Jibu ni kwa kuyafanya, Aaah kumbe! Ili nisilaaniwe inabidi niyafanye yale Bwana aniamuruyo, unaweza kwenda mbali kidogo kwa kusema ya kwamba, ili mtu apokee Baraka ni lazima, ndio nasema ni lazima namaanisha ya kwamba sio ombi!, NASISITIZA NI LAZIMA ASOME NA KUTENDA SAWA SAWA NA NENO LA MUNGU.
Sasa kwa kuwa neno la Mungu lina umuhimu sana basi Musa alipokufa tu, Mungu aliendelea kumkumbusha hata Yoshua juu ya umuhimu wa kuzingatia maneno yake, ili asitawi katika maisha yake na kuepuka laana kabisa, sasa unaweza ukajua kwamba Baraka zilizomiminika kwa wana Israeli zinatokona moja kwa moja na kutunza na kufanya maagizo ya BWANA Mungu, soma mwenyewe Kumbukumbu 28:1-14.
Sasa ukisikia Mungu anazungumza jambo na wewe halafu unakaidi kutenda, utakuwa unatafuta matatizo wewe mwenyewe, yaani ukisikia Mungu anasema utalaaniwa kwa kutokuweka imara torati yake, inamaanisha kuwa utalaaniwa kweli kweli, sasa basi wewe ukielewa hivyo tu, unatakiwa uweke imara torati ya BWANA Mungu wako ili ubarikiwe na usilaaniwe. Kumbuka kanuni yetu ya muhimu kabisa na rahisi sana itakayokuwezesha kupokea Baraka “SOMA NENO,TAFAKARI NENO,TENDA NENO”.  



  1. UTAKUFA KIROHO NA KIMWILI
Labda nianze kwa kukuweka sawa ya kwamba, kanuni ni kwamba ukitaka kufa kimwili basi anza kwanza kuua Roho, na ukitaka kufanikiwa kimwili anza kutafuta kufanikiwa kiroho kwanza, ninajua kwa sasa unaweza usielewe namaanisha nini. Lakini kwa kuwa Roho Mtakatifu ni mwema mimi ninajua ya kwamba atakupitisha kwenye shule hii kiurahisi kabisa. Haya sasa je! Ndugu upo tayari tufundishwe sote na Roho Mtakatifu?
Haya tuanze shule yetu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu sasa kwa kusoma 3 yohana 1:2, utakuta maneno yafuatayo “mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo”, haya sasa! Najua umeanza kupata picha kidogo kwamba namaanisha nini, Ni wazi kabisa kwamba utafanikiwa kwa kadiri au kwa kiwango cha mafanikio ya roho yako, sasa kama roho yako inafanikiwa kidogo na mwili pia utafanikiwa kidogo, kama roho yako itafanikiwa sana na mwili pia kadhalika. Na tena kama roho yako itaishi na mwili pia utaishi, sasa basi! ujue kwamba roho yako ikifa na mwili wako utakufa tu.
Hebu sasa tuyaangalie maneno ya kitabu cha Mathayo 4:4 ambayo yanasema “naye akajibu akasema, imeandikwa , mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.”  Sasa najua utaelewa ya kwamba kuishi kwako kutatokana na jinsi ulivyolijaza neno la Mungu ndani yako, kadhalika kufa kwako kutatokana na kutolijaza neno la Mungu ndani yako.
Hivi unafikiri Yesu asingelikuwa na neno ndani yake angemjibu kwa kusema imeandikwa! Hebu jiulize imeandikwa wapi? Halafu fikiri kwa nini Yesu alisema hakuja kuitangua torati bali kuitimiza. Sasa utaelewa ya kwamba mwana mpendwa wa Mungu, yaani Yesu mwenyewe aliishi kwa kuzingatia na kutenda neno, sasa kwa nini wewe usitende neno?
Ndugu yangu mpendwa, mimi ninakushauri ujitahidi kujua neno la Mungu, ili shetani asikutishe na kukuletea uongo wake kabisa. Kwa mfano akikujaribu katika masomo ya kwamba utafeli, wewe ungali ukijua neno la Mungu umwambie kwa ujasiri wote ya kwamba “ imeandikwa kwenye kumbukumbu 28:13, ya kwamba BWANA atanifanya kuwa kichwa na wala sio mkia;………., kwa hiyo ni lazima nifaulu katika jina la Yesu”, akikujaribu kwenye Ndoa umwambie  imeandikwa katika mithali 18:22 ya kwamba “apataye mke apata kitu chema; naye ajipatia kibali kwa BWANA,  kwa hiyo mimi nimepata mke au mume mwema kabisa kabisa katika jina la Yesu”, akikwambia wewe ni maskini umwamie “imeandikwa katika wafilipi 4:19 ya kwa Mungu atanijaza kila nachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake, kwa hiyo mimi ni tajiri katika jina la Yesu”. Sasa kwa  nini uteseke na Yesu yupo? Tena anakupenda na kukujali?, wewe jitahidi tu kusoma neno na kumwomba yeye, naye hakika atakusaidia.
Hebu na tusome kwa kutafakari Mithali 4:20-22, Isemayo “mwanangu, sikiliza maneno yangu; tega sikio lako, uzikie kauli zangu. Zisiondoke machoni pako ; uzihifadhi ndani ya moyo wako. Maana ni UHAI kwa wale wazipatao, na afya ya mwili wao wote.”, nadhani umejionea mwenyewe hilo neno ni UHAI kwa wale wazipatao, na afya ya mwili wao wote. Sasa ni lazima uelewe kwamba mithali hii ya sulemani ina maana kubwa sana kwako mtu wa Mungu, ya kwamba ni lazima uyasikilize maneno ya Mungu, halafu utege sikio usikie kauli za BWANA, halafu tena zisiondoke machoni kwako kabisa bali uzihifadhi, hebu jiulize, je uzihifadhi wapi?, Ni rahisi kabisa uzihifadhi ndani ya moyo wako, Kwa tafsiri nyingine uhai wako unategemea neno la Mungu.
Ndugu yangu usisahau kanuni yetu ya mambo yote! SOMA NENO, TAFAKARI NENO, TENDA NENO, ili upate uhai wako na usife kwa kukosa kuifahamu kweli ya Mungu wetu.



  1. UTATENDA DHAMBI
Soma mwenyewe Zaburi 119:11, ambapo neno la Mungu linasema “moyoni mwangu nimeliweka neno lako, nisije nikakutenda dhambi”, ngoja tujiulize kwa pamoja kabisa, hivi ni kwa nini neno katika zaburi halikusema  ya kwamba, “moyoni mwangu nimejaza maombi nisije nikakutenda dhambi, au moyoni mwangu nimezijaza sifa zako nisije nikakutenda dhambi, au moyoni mwangu nimejaza ibada  nisije nikakutenda dhambi, au “moyoni mwangu ……………………………. Nisije nikakutenda dhambi?”
Jibu ni rahisi kabisa mtu wa Mungu ni vema ufahamu ya kwamba neno ni msingi wa kila kitu katika maisha yako, ukitaka kuomba vizuri lazima ujue neno linasemaje juu ya maombi (yohana 15:7), tena ukitaka kusifu vizuri ni lazima ujue neno linasemaje kuhusu sifa (waebrania 13:15), tena ukitaka ibada nzuri ni lazima ujue neno la Mungu lasemaje kuhusu ibada (yohana 4:23-24), tena ukitaka …………… tafuta kwanza neno la Mungu linasemaje kuhusu ………….. na utende.
Sasa ni lazima umwombe Roho Mtakatifu akusaidie na wewe uweze kuliweka neno la Mungu ndani yako ili tu usije ukamtenda Mungu dhambi, ndio eeh! Lazima umwombe Roho Mtakatifu akusaidie kwa sababu vita iliyopo juu ya kusoma neno ni kubwa sana, Shetani hataki kabisa wewe ujue neno kwa sababu atakukosa katika orodha yake ya kwenda jehanamu.
Ndugu jitahidi ujue neno la Mungu ili uepuke mshahara wa dhambi ambao ni mauti (warumi 6:23), sasa kama unataka mauti, kazi ni rahisi sana, wewe jitahidi kutojua neno la Mungu ili utende dhambi. Ila kama unataka uzima wa milele, pia kazi rahisi SOMA NENO, TAFAKARI NENO, TENDA NENO.




NINI FAIDA YA KUSOMA,  KUTAFAKARI NA KUTENDA NENO?
1.      YESU ATAKUOMBEA
Ukisoma katika kitabu cha Yohana 17:8-9 utakuta maneno yafuatayo “kwa kuwa maneno uliyonipa nimewapa wao; nao wakayapokea, wakajua hakika ya kuwa nalitoka kwako, wakasadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Mimi nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako ”, Sasa unaweza ukatambua ya kwamba ukilipokea neno la Mungu basi Yesu  mwenyewe atakuwa akikuombea, ukiangalia katika mistari ya kwanza kabisa ya mlango huu wa 17 utagundua ya kwamba Yesu aliomba maombi haya katika wakati ambao alikuwa anakaribia kabisa kuteswa na kufa kwa ajili ya wanadamu wenye dhambi.
Sasa unaweza ukajiuliza ni kwa nini asingeomba tu kwa ajili ya ulimwengu mzima katika maombi yake haya!, bali akaanza kwa kusema maneno uliyonipa nimewapa wao nao wakayapokea, halafu akasema katika mstari wa 9 mimi nawaombea hao. Sasa namwomba roho mtakatifu ayafungue macho yako upate kuelewa na maandiko (luka 20:45), ya kwamba kama hutaki neno Yesu hawezi kujiangaisha na wewe, ila kama ukijaza neno lake ndani yako; uelewe kabisa ya kwamba atakuombea.   
 ukiendelea tena mbele kidogo na kusoma kitabu cha yohana 17:14-15 utakuta Yesu akiendelea kusema “mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na Yule mwovu. ” naomba uelewe kwamba, Mambo haya sio ya kawaida kawaida, ukae ukijua ya kwamba ukilitambua neno la Mungu wa kweli ni lazima uchukiwe!, kama hutaki kuamini hebu anza leo kuishi sawa na neno la Mungu. Halafu uone kama hujachukiwa na wale rafiki zako uliokuwa ukienda nao disco, tena kama hujachukiwa na Yule uliyekuwa unazini nae kabla ya kujua neno, halafu kama hujachukiwa na Yule ulikuwa ukishinda nae bar, tena zaidi sana kama hujachukiwa na Yule ulikuwa ukienda nae kwa mganga ili umfanyie madawa mumeo. Mimi nakwambia utachukiwa sana; lakini ukae ukitambua ya kwamba thamani yako itapanda kwa kuwa Yesu mwenyewe atakuombea, halafu Yule mwovu hatakuweza tena katika jina la Yesu kristo wa nazareti aliye hai.
Je unataka Yesu mwenyewe akuombee kila mara?, usisahau ya kwamba kanuni yetu ambayo Yesu ametupa sisi kupitia kwa Roho Mtakatifu ni ndogo tu! SOMA NENO, TAFAKARI NENO, TENDA NENO.



2.      UTAIJUA KWELI, KISHA UTAKUWA HURU
Ukisoma katika kitabu cha Yohana 8:31-32 utakuta maneno haya “ basi Yesu akawaambia wale wayahudi wasiomwamini, ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaijua kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru”,  tena  ukisoma katika kitabu cha Yohana 17:17 utakuta maneno yafuatayo “uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli”
Bila shaka kutokana na maneno tuliyosoma utakuwa umepata kuelewa ya kwamba; neno la Mungu ndiyo kweli itakayokusaidia kiroho na kimwili. Ukitaka kuwa huru kabisa katika mambo yote maishani mwako, kanuni ni ndogo tu SOMA NENO,TAFAKARI NENO, TENDA NENO.
Sasa kama hutaki kuishi katika kweli maana yake unataka uwe katika vifungo, na ninakuhakikishia shetani hatakuachia hata siku moja kwa kwenda kwako kanisani pekee, au kuimba kwaya pekee, au kuwa shemasi pekee, au hata kuwa mwinjilisti au mchungaji. Shetani atakuachia na utakuwa huru kweli kweli pindi tu utakapoijua kweli ambayo ni neno la Mungu wa mbinguni (biblia yaani maandiko matakatifu).
Mimi nakushauri ujitahidi kwa kadiri uwezavyo ili tu uwe msomaji wa neno, halafu usiishie tu kulisoma bali ulitafakari, zaidi sana ukalitende. Kisha upokee uhuru wako katika mambo yote maishani mwako.



3.      UTAFANIKIWA NA KUSITAWI  SANA
Hii ni wazi kabisa kwamba; mafanikio yako na usitawi wako, vipo kwenye neno la Mungu, unaweza usielewe kirahisi sana lakini najua Roho Mtakatifu atakusaidia uelewa wako na Yesu atafungue macho yako ili uone anakuwazia nini pindi tu upatapo kulijua neno lake. Sasa tukisoma katika kitabu cha Yoshua 1:8 utakuta Mungu anamwambia Joshua ya kwamba “kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali YATAFAKARI maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia KUTENDA sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; ndipo UTAKAPOIFANIKISHA njia yako, kisha ndipo UTAKAPOSITAWI sana.
Lazima uelewe ya kwamba mafanikio yako yote yataletwa na wewe kufahamu neno la Mungu, bila neno hakuna mafanikio. Mimi nakwambia ya kwamba Mungu anaangalia neno lake alitimize (yeremia 1:12b), halafu anataka umpelekee hoja zenye nguvu, halafu anataka ueleze mambo yako upewe haki yako (isaya 43:26).
Hivi unafikiri unaweza kudai haki usiyojua kama ni yako? Au unaweza kuomba kitu pasipo na kujua kama kipo? Au? Au? Najua maswali ni mengi sana, tena mengine na wewe unayo. Lakini neno la Mungu limeweka wazi kabisa suala hili; kwamba Mungu huliangalia neno lake ili alitimize (yeremia 1:12b), sasa kama huna neno la Mungu unafikiri ni kitu gani kitatimizwa kwako?
Lazima uelewe kwamba mafanikio yako yanakuja kwa kulifahamu neno la Mungu, kwa mfano; unataka mke mwema, mithali 18:22 ipo wazi kabisa kwamba apatae mke apata kitu chema. Sasa wewe unapokwenda kwa Mungu kuomba pasipo kujua neno hili, ujue ya kwamba maombi yako yatakuwa kelele kwa Mungu, kwa sababu Mungu anaangalia neno lake ili alitimize, unataka mafanikio yako ya mbeleni yawe mazuri, Isaya 45:11  ipo wazi kabisa Mungu anataka umuagize juu ya mambo yanayokuja, sasa wewe unapokwenda kwa Mungu kuombea maisha yako yajayo pasipo na kujua neno hili; ujue utapiga kelele bure kwa Mungu, halafu yeye ashakwambia anaangalia neno lake ili alitimize, si hayo tu neno la Mungu lina majibu ya kila unachokifahamu hapa chini ya jua.
Kwa hiyo unataka kufanikiwa na kusitawi kanuni tuliyopewa ni ndogo tu; SOMA NENO,TAFAKARI NENO ,TENDA NENO. Vinginevyo usahau tu kuhusu mafanikio kwa sababu shetani atakuwa amekufunga kisawasawa na kwa kuwa anachukia usitawi wako hutafanikiwa. Lakini kwa jina la Yesu kupitia Roho Mtakatifu wake ambao leo, wamekupa wewe kibali cha kusoma kitabu hiki ninamuamuru shetani aachie fahamu zako ili upate kupokea kile mungu anachokuwazia (yeremia 29:11) katika jina la Yesu kristo wa nazareti aliye hai.



4.      UTAMSHINDA SHETANI
Hebu tujiulize swali hili kwa pamoja kabisa, Je utamshindaje shetani? Ni rahisi kabisa ukisoma katika kitabu cha waefeso 6:10-20, utakuta mtume Paulo anawaandikia watu wa efeso kwamba wanatakiwa wawe hodari katika bwana na katika uweza wa nguvu zake, kisha wavae silaha zote za Mungu ili waweze kuzishinda hila za shetani; Kwa maana kushindana kwetu si juu ya damu na nyama bali juu ya falme na mamlaka. Sasa ukiangalia kuanzia mstari wa 14 mpaka wa 20 utakuta zimerodheshwa silaha za kuweza kumpinga shetani na kumshinda kabisa kabisa. Mimi nakushauri uzisome na kuangalia kutenda sawa sawa na neno hili la Mungu ili uweze kumpinga shetani
Kwa hiyo ukisoma Waefeso 6:17b  utakuta maneno haya “na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu” kumbuka kuanzia mstari wa 14 mpaka wa 20 zilikuwa zinazungumziwa silaha za Mungu, sasa neno ni upanga wa Roho; kwa maana nyingine neno linao uwezo wa kumkata kata shetani na serikali yake yote ya kuzimu.
Sasa kama neno ni upanga na wewe hujui neno, tena hutaki kulijua kabisa kabisa, na hata ukipata neema ya kulijua hutaki kulitumia (kulitenda) maishani mwako, unategemea nini?, jibu ni rahisi kabisa nalo ni!, utake usitake ni lazima shetani atakushinda kwa sababu akiangalia rohoni mwako kama kuna upanga utakaoweza kumpinga hauoni, Na asipouna anakuangamiza wewe ili usije ukajua neno (upanga wa Roho) halafu ukamteketeza.
Nikushauri tu ndugu yangu mpendwa ya kwamba, Upanga huu wa Roho hauna gharama yoyote kuupata, ingawa shetani anajaribu kukurubuni usiutafute na kuutumia. Amua hivi sasa kumpokea Yesu kwanza kama bado hujampokea kwa kufuatisha sala ambayo utaikuta mwishoni mwa kitabu hiki, kisha umwombe Yesu wewe mwenyewe kwa kinywa chako akusaidie kupitia Roho Mtakatifu, uweze kuelewa maandiko na upate hamu ya kuijua kweli ili uwe huru, na umshinde shetani kabisa kabisa. 
 


5.      UTAPATA NGUVU YA MUNGU
Katika 1Wakorintho 1:18, neno la Mungu linasema “ kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu za Mungu.” Sasa usije ukatafsiri kama wengi wanavyotafsiri, maana wengi hudhani imeandikwa hivi, “kwa sababu neno msalaba” hapana haijaandikwa kwa sababu neno msalaba, bali imeandikwa kwa sababu neno la msalaba, je neno la msalaba ni lipi? Ukisoma katika kitabu cha 2 wakorintho 4:3 utakuta neno hili limejaribu kuelezewa kwa namna nyingine kwamba, “lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea”. Najua pamoja na kutambua kwamba neno la Mungu kwa sehemu nyingine limeelezwa kama injili, bado kuna wengine hawajaelewa kabisa ni nini ninachokizungumzia hapa, haya hebu tuangalie warumi 1:16 ili tuone habari ya injili hii, maneno ya Mungu yanasema “kwa maana siionei haya injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa myahudi kwanza, na kwa myunani pia” 
Sasa najua umeanza kupata picha ya kwamba, neno la msalaba ni nguvu za Mungu kwetu sisi tunaookolewa, kwa maana nyingine kama hujaokoka huwezi kuwa na hizi nguvu za Mungu, kwa sababu pia husomi neno. Najua wengine bado wanajiuliza maswali mengi juu ya uhusiano wa neno la Mungu, neno la msalaba na injili, sasa ngoja Roho mtakatifu atusaidie kutupa majibu, hivi kuna mtu ashawahi kuubiriwa injili kwa kutumia kitabu cha siasa? Au basi kitabu cha hisabati? Au basi kwa kutumia gazeti? Au kitabu cha hadithi? Au? Au? Au?.............., najua jibu lake ni HAPANA! Haya sasa tujiulize tena, hivi mtu ashawahi kuubiriwa injili kutumia neno la Mungu yaani maandiko matakatifu au kama inavyofahamia Biblia?, jibu lake ni rahisi sana, au wewe unafikirije ndugu msomaji?, ila mimi nadhani jibu lake ni! NDIO watu huubiriwa injili kwa kutumia neno la Mungu yaani Biblia.
Sasa utakubaliana na maneno ya mtume Paulo katika 1wakorintho 1:18 kwamba, utapata nguvu za Mungu kwa neno la msalaba, lakini hakuishia hapo ukiliona neno la msalaba ni upuuzi basi utapotea. Sasa amua leo, je unataka kupotea au kupata nguvu za Mungu! Mimi binafsi nakushauri uamue kupata nguvu za Mungu kwa kujua neno la msalaba. Na usiishie tu kulijua bali ulitafakari na kisha ulitende, nakuhakikishia ya kwamba utaziona nguvu za Mungu katika jina la Yesu.



6.      UTAPATA MWANGAZA KATIKA MAISHA YAKO
Katika Zaburi 119:105 maneno ya Mungu yanasema hivi “neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu”, je taa yako na mwanga wa njia yako ni nini?, najua jibu unalo wewe mwenyewe, pengine ni waganga, au pombe, au uongo au chochote ambacho unasikia Roho Mtakatifu akikukumbusha ndani ya roho yako. Lakini katika maneno ya zaburi taa na mwanga wa mtu wa Mungu ni neno la Mungu, sasa kama wewe umeokoka halafu huna taa hii inayokuletea mwanga katika njia zako basi una bahati mbaya sana. Ila mimi nikushauri katika jina la Yesu, uanze leo kuiwasha taa ya neno la Mungu maishani mwako ili upate mwanga katika mambo yako yote. Anza sasa,! kusoma, kutafakari na kutenda sawa na neno la Mungu, bado hujachelewa!
 ukisoma tena katika kitabu cha yohana 1:4-5 utakuta iimeandikwa “Ndani yake ndimo ulikuwamo uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.”, unaweza ukajihoji ndani ya kitu gani kulikuwamo uzima, uliokuwa nuru ya watu?, ni rahisi kabisa. Ni ndani ya neno ndimo kulikuwamo uzima, nao uzima ulikuwa nuru ambayo haikuwezwa na giza kabisa. Ndugu yangu hebu tafuta huo uzima katika neno, ili upate nuru na maisha yako yabadilike kabisa kabisa, ili nawe upate mwangaza katika maisha yako bado hujachelea anza sasa kutenda sawa sawa na maandiko. 
tena ukisoma katika kitabu cha waefeso 1:18-19 utakuta maneno kwamba “macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake;”, haya sasa macho yako yatatiwa nuru gani zaidi ya neno?, hakuna nuru popote zaidi ya neno la Mungu, ukiangalia vizuri katika waefeso 1:18-19 utagundua ya kwamba, huwezi kujua tumaini la wito wake bila nuru ambayo ni neno, tena huwezi kujua utajiri wa urithi wake bila kutiwa nuru itokanayo na neno, tena huwezi kujua ubora wa uweza wake ndani yako bila kutiwa nuru itokanayo na neno; tena huwezi lolote lile unalolijua bila neno.
Kwa hiyo sasa neno ni msingi wa kila kitu kwa kila mwanadamu, ukitaka mafanikio na usitawi soma neno, hutaki mafanikio na usitawi acha kusoma neno. Lakini mimi nimepata mafanikio mengi na makubwa ambayo Yesu amenitendea mara tu baada ya KUSOMA NENO, KUTAFAKARI NENO NA KUTENDA SAWA SAWA NA NENO.




KIPI BORA! FAIDA AU HASARA?
Mmh! Mimi ntashangaa sana kama utachagua hasara ambazo zipo nyingi kuliko hizo nilizoziandika hapo, Roho Mtakatifu ameamua tuziangalie hasara hizo chache kwa undani. Ila haimaanishi kwamba zipo hasara hizo tu, bali hizo ni chache alizoamua kutufundisha, hivi kweli unaweza kuamua kuchagua kuangamia kiroho na kimwili? Au kutopata majibu ya maombi yako? Au kulaaniwa? Au kufa kiroho na kimwili? Au kutenda dhambi?, ninajua utakuwa umeitikia HAPANA. Sasa basi mbona bado hutaki kusoma, kutafakari na kutenda neno?.
Haya sasa je! Upo tayari kupata faida zinazotokana na kusoma, kutafakari na kutenda neno?. Mmh Asante sana kwa jibu lako zuri! Sasa wewe ambaye upo tayari kuombewa na Yesu, tena kuijua kweli ili uwe huru, halafu ufanikiwe na kusitawi, tena umshinde shetani, na tena upate nguvu za Mungu, kisha upate mwangaza katika maisha yako. Mbona hutendi sawa na maagizo ya neno la Mungu?
Mimi nakushauri leo uchague faida, na umpokee Yesu. Lakini pia ukichagua hasara shauri yako mwenyewe! Kwa sababu Yesu ameamua kukufundisha yeye mwenyewe kupitia Roho wake mtakatifu, katika kitabu hiki. Mpokee Yesu leo upate faida mpendwa. 




HITIMISHO
“basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu”, waefeso 3:20, ninapenda kumshukuru Mungu kupitia mwanae Yesu kristo kwa msaada wa Roho Mtakatifu wake kwa kuniwezesha kuandika kitabu hiki ambacho amekiweka mkononi mwako ili kiwe msaada wako wa kiroho.
Ndugu mpendwa mimi binafsi nakushukuru kwa kutoa muda wako mwingi sana na ulio na dhamani kubwa na kuamua kukisoma kitabu hiki, lakini napenda nikwambie ya kwamba Mungu amekuwezesha wewe kusoma kitabu hiki kwa mpango kamili kabisa, kwa kuwa yeye anakuwazia mema siku zote (yeremia 29:11), halafu alijua ya kwamba leo atakufungua macho ili upate kuelewa maandiko yake (luka 24:45), sasa mimi nikushauri kama ulikuwa hujaokoka ni vema uchukue uamuzi leo wa kumpokea Yesu kama bwana na mwokozi wako (yohaha 3:16-17, warumi 10:10,13 na matendo 4:12) kwa kusali sala fupi itakayofuata baada ya hitimisho hili huku ukimaanisha, najua unaweza ukajiuliza swali hili, hivi ni kwa nini mimi ninakushauri wewe uokoke? Jibu ni rahisi sana ndugu yangu, mimi ninakushauri uokoke kwa sababu hutaweza kupata kibali cha kuyaelewa maandiko na kuishi maisha ya mafanikio na usitawi bila msaada wa Roho Mtakatifu, na Roho Mtakatifu hawezi kukaa ndani yako ukiwa bado ungali mwenye dhambi (1 wakoritho 3:16-17), hebu chukua hatua sasa ya kumpokea Yesu na uanze kuona mafanikio na usitawi wako, hujachelewa chukua uamuzi wa kuokoka hivi sasa; Kwa kutafuta mahali penye utulivu na kusali sala ifuatayo kwa sauti kabisa huku ukimaanisha, tambua ya kwamba Yesu yupo nawe hapo ulipo, halafu tena yupo tayari kukusamehe na kukupokea kisha akufanye kiumbe kipya.




SALA YA TOBA
Ndugu yangu Sali sala ifuatayo kwa sauti kabisa huku ukimaanisha, haya sasa mpendwa hebu sema maneno yafuatayo;-
“BWANA YESU, NINAKUJA MBELE ZAKO HIVI SASA. NIMESIKIA SAUTI YAKO KUPITIA NENO LAKO TAKATIFU, YA KWAMBA, NIZIACHE DHAMBI ZANGU ZOTE, NA NIKUFUATE WEWE YESU, ILI UNIBADILISHE NIWE KIUMBE KIPYA, NIMEAMUA KWA DHATI KUTOKA NDANI YA MOYO WANGU, KUZIACHA DHAMBI ZANGU ZOTE NA KUKUFUATA WEWE. NISAMEHE DHAMBI ZANGU ZOTE NA USIZIKUMBUKE KABISA KAMA ULIVYOSEMA KATIKA KITABU CHA ISAYA 43:25, NISAFISHE KWA DAMU YAKO NA UNIFANYE KIUMBE KIPYA. NIPE NA ROHO MTAKATIFU WAKO ILI ANISAIDIE KUISHI VEMA KATIKA WOKOVU, SIKU ZOTE ZA MAISHA YANGU, AMEN.”
Hongera sana kwa uamuzi uliouchukua hivi leo, ninapenda kukuhakikishia ya kwamba Mungu kupitia mwanae Yesu kristo amekusamehe dhambi zako zote, hajakusamehe dhambi baadhi tu, bali dhambi zote. Usiogope kusema mbele za watu ya kwamba umeokoka, lakini pia ninakushauri utafute kanisa lolote la kiroho ambalo utasikia Roho Mtakatifu ndani yako akikuruhusu kwenda, na ujumuike nao katika ibada na uwaeleze ya kwamba umeokoka na unahitaji msaada zaidi wa kiroho nao kwa jina la Yesu Kristo wa nazareti aliye hai watakusaidia ili uishi maisha mazuri hapa duniani na kisha utapata uzima wa milele
Lakini ngoja nikupe siri hii, kwa kuwa umeokoka vita yako na shetani itakuwa kubwa sana. Sasa basi hebu soma waefeso 6:10-20 kwa kutafakari ili uzijue silaha ambazo zitakusaidia wewe kupambana na shetani. Na ukizishika silaha hizo vizuri kwa msaada wa Roho Mtakatifu, ninakuhakikisia ushindi kwako ni lazima.
Vitu vya Muhimu sana kwako wewe uliyeokoka ni: neno(yoshua 1:8), ibada(yohana 4:23-24) na maombi (wafilipi 4:6 na yohana 15:7)

NDUGU MPENDWA, UBARIKIWE NA BWANA YESU. NINAKUPENDA!

MWISHO WA SOMO

By Clement Emmanuel of Rij Company limited

No comments:

Post a Comment